18 Oktoba 2025 - 23:23
Kuwanyang’anya silaha wamiliki halali wa ardhi ya Palestina ni kuwapendelea kabisa wavamizi / Umuhimu wa Kuamka kwa dhamiri za tawala za Kiarabu

Dkt. Rabhiy Halloum amesisitiza kuwa uamuzi wa kweli wa kisiasa na kuamka kwa dhamiri za nchi za Kiarabu ndiko kutakakoamua mustakabali wa ukombozi wa Palestina na kulinda amani ya kudumu katika eneo lote la Mashariki ya Kati.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dkt. Rabhiy Halloum, Mwanadiplomasia wa zamani wa Palestina aliyehudumu kama balozi katika nchi kadhaa zikiwemo Uturuki, Falme za Kiarabu, Brazil na Indonesia, na pia mwanachama wa zamani wa harakati ya Fatah na Baraza la Kitaifa la Palestina, amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA kwamba:

“Kuwanyang’anya silaha wamiliki halali wa ardhi ya Palestina ni kitendo cha upendeleo wa wazi kwa wavamizi wa Kizayuni. Wenye haki ya kujihami ni watu wa Palestina, si wavamizi wanaonyakua ardhi yao.”

🔸Kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni

Dkt. Halloum amesema kuwa utawala wa Kizayuni hauna uwezo wa kupigana vita vya muda mrefu, bali huchagua vita vya haraka na vya muda mfupi kwa malengo ya muda maalumu. Kwa mujibu wake, Israel hupanga malengo yake, ratiba ya utekelezaji, na mipango ya kijeshi kwa kipindi kifupi, na hukubali kusitisha mapigano pale inapofikia baadhi ya malengo yake ya muda mfupi.

Amesisitiza kuwa usalama wa kudumu wa eneo hili hautapatikana isipokuwa kwa kuamka kwa dhamiri za tawala za Kiarabu, kujitolea kwao kutekeleza Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa Nchi za Kiarabu, na kushirikisha wananchi wao katika maamuzi ya kisiasa, kiuchumi, na kibinadamu.

🔸Kuhusu mpango wa kuunganisha Ukingo wa Magharibi

Amesema kuwa serikali ya Israel, chini ya ushawishi wa viongozi wenye misimamo mikali kama Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich, imeharakisha kuidhinisha mpango wa kuunganisha Ukingo wa Magharibi na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, jambo linalojumuisha kuhamisha zaidi ya walowezi 800,000 kwenda eneo hilo.
Kwa maoni yake, hatua hii ni mwendelezo wa sera za upanuzi wa utawala wa Kizayuni ambazo hata viongozi wa Marekani, akiwemo Donald Trump, walikuwa wakizipa baraka kwa malengo yao ya kisiasa.

🔸Kuhusu madai ya kuondoa silaha kwa Hamas na makundi ya mapambano

Dkt. Halloum amesisitiza kwamba yeyote anayependa haki anapaswa kwanza kupendekeza kuondolewa silaha kwa wavamizi wa Kizayuni, si kwa watu wanaolinda ardhi yao halali.
Amesema:

“Mikataba na sheria za kimataifa, ikiwemo Kifungu cha 7 cha Katiba ya Umoja wa Mataifa, vinatoa haki kwa kila taifa kujilinda kwa kila njia, ikiwemo kutumia silaha, dhidi ya uvamizi au ukaliaji wa kigeni.”


🔸 Kuhusu hatma ya taifa la Palestina na mipango ya ‘Toni Blair’

Dkt. Halloum amesema kuwa watu ndio chanzo halisi cha mamlaka, na viongozi wa Palestina wanapaswa kuchaguliwa kupitia uchaguzi huru na wa haki.

“Hakuna serikali yoyote isiyo ya kisheria au isiyochaguliwa na wananchi inayoweza kudai uhalali wa kuwaongoza Wapalestina,” amesema.

🔸Kuhusu kufunguliwa kwa kivuko cha Rafah

Amefafanua kuwa hatua ya Israel kufungua kivuko cha Rafah si ishara ya huruma, bali ni jaribio la kukwepa kutengwa kimataifa na kufunika uhalifu wa vita dhidi ya watu wa Palestina katika Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Kwa jumla, Dkt. Rabhiy Halloum amesisitiza kuwa uamuzi wa kweli wa kisiasa na kuamka kwa dhamiri za nchi za Kiarabu ndiko kutakakoamua mustakabali wa ukombozi wa Palestina na kulinda amani ya kudumu katika eneo lote la Mashariki ya Kati.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha